Hafla ya 47 ya Kufuzu kwa Wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Egerton, Njoro, Kenya Ijumaa tarehe 27 Oktoba, 2023 Hotuba ya Mwenyekiti wa Halmashauri inayosimamia Chuo, Balozi Daktari Hukka Wario, PhD, CBS
Bwana Chansela wa chuo hiki, Daktari Narendra Raval Waziri wa Elimu, Mheshimiwa Ezekiel Machogu,
Katibu katika wizara, Idara ya Elimu ya juu na Utafiti, Daktari Beatrice Inyangala,
Waheshimiwa Mawaziri wengine, Maseneta, Wabunge na viongozi wa tabaka mbalimbali kutoka serikali kuu na serikali ya kaunti walioko hapa.
Nataka kuchukua nafasi hii kumtambua kwa heshima Seneta wa Marsabit, Mheshimiwa Mohamed Chutè, ambaye pia ni seneta wangu na rafiki yangu, yupo hapa na sisi leo, kusherehekea kufuzu kwa mwanawe Nur Mohamed Chute leo anayehitimu katika masomo ya udaktari na upasuaji. Karibu mheshimiwa seneta. Asante kwa kuja na kujumuika nasi. Jihisi, kama uko nyumbani.
Wanachama wa halmashauri inayosimamia chuo hiki, ambayo mimi ndiye mwenyekiti,
Naibu Chansela, na mkuu wa chuo hiki, Profesa Isaac Kibwage, manaibu wake Profesa Richard Mulwa na Profesa Bernard Aduda,
Baraza la utawala wa chuo, Maprofesa na wahadhiri wote, na wafanyi kazi wote wa chuo.
Nataka kuwatambua kwa njia ya kipekee, wazazi wa wanafunzi wanaofuzu leo, na marafiki wao waliofika hapa,
Chama cha wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Egerton, wanafunzi wote wanaoendelea na masomo, wanachama wa halmashauri ya wale waliofuzu hapo mbeleni kutoka chuo hiki, yaani Aluminai, Marafiki wa chuo kikuu cha Egerton, karibuni sana, na hamjambo? Hamjambo tena?
Leo, maneno yangu ni manane.
- Neno la kwanza in kuwapongeza, kuwashukuru na kuwapa hongera wanafunzi wote wanaofuzu hivi leo, kwa kufikia kilele cha masomo baada ya kusoma kwa bidii kwa miaka mingi ya kujitolea.
- Ujumbe wangu wa pili. Hamngalifuzu bila usaidizi wa wazazi, walimu hapa chuoni, wafadhili na marafiki wasaidizi. Kwa hivyo nina jukumu la kuwashukuru hawa wote.
- Ujumbe wangu wa tatu. Hii ni siku ya furaha. Siku ya kipekee katika maisha yenu. Mnapaswa kuisherehekea pamoja na wazazi na marafiki wenu
wote, na sisi sote tulioko hapa. Basi mnionyeshe ya kwamba mnafuraha kwa kuinua na kutupa juu kofia ya kufuzu, kwa shangwe na vigelegele. Hebu tuone…moja…mbili…tatu… asanteni sana.
- Tunafurahi na nyinyi ya kwamba mmepata elimu. Hata ingawa elimu ni kitu kinachaoendelea katika maisha yetu yote, kutoka kuzaliwa hadi kufa, mmepata elimu ya kujivunia. Lakini ukiwa na bahati ya kupata elimu ya juu, ujue ya kwamba, si kila Mkenya amekua na bahati ya kusomea chuo kikuu. Kwa hivyo huu si wakati wa kujigamba jinsi
umesoma chuo kikuu, bali ni wakati wa kunyenyekea na kuhudumia wale ambao hawajabahatika kama wewe.
- Wewe mwanafunzi unayefuzu leo, nisikilize, niazime masikio yako yote mawili kwa dakika moja tu. Wewe ni mwangaza; elimu yako ya juu ndio imekupa mwangaza na ufahamu zaidi ya wale hawajasoma kama wewe. Wewe ni mshumaa au taa inayotoa mwangaza. Hata katika biblia takatifu, kitabu cha Marko , sura ya 4, kifungu cha 21 hadi 23, imeandikwa “huwezi kuwasha mshumaa ama taa
na ukaiweka chini ya meza”. Inakubidi uiweke juu ya meza, ili chumba kizima kipate mwangaza. Basi katumieni elimu yenu kuwapa wanavijiji, watu wanaoishi karibu nanyi, mwelekeo na ufahamu wa maisha bora zaidi; ili hata hawa
wafaidike na elimu yenu. Kila mmoja wenu akifanya hivyo, kwa jumla, taifa litafaidika na kutakuwa na maendeleo zaidi.
- Ujumbe wangu wa sita ni mawaidha kuhusu kujiajiri au kuajiriwa kazi. Kwa kawaida mnachukua kazi yoyote inayojitokeza, kwa sababu kazi ni haba na
hazipatikani kwa urahisi. Lakini ukipata kazi fulani, si lazima ukae papo hapo mpaka uzeeni. Nawahimiza mjiendeleze na masomo zaidi, mpate ujuzi mapya na uzoefu ili muweze kubadilisha kazi kwa ile inayokufaa, inayokufarahisha zaidi na inayokulipa mshahara bora na wa kukuridhisha.
- La saba; nataka kuchukua nafasi hii kushukuru Chansela wetu, Daktari Narendra Raval kwa kulipia gharama ya karo ya chuo kwa wanafanzi kumi wanaosoma hapa, kwa miaka yote minne hivi. Hawa
ni wanafunzi waliokua na mahitaji zaidi. Pia Chansela aliwazawadi wanafunzi walioshinda katika shindano la uandishi almaarufu “Chancellor’s Essay Writing Competition”. Zawadi ya kwanza ilikua ya shillingi 50,000, ya pili shillingi 40,000, ya tatu shillingi 30,000, ya nne shillingi 20,000 na ya tano shillingi 10,000; jumla ya pesa ziliozawadiwa makala hayo ilikua shillingi elfu mia mbili na hamsini (250,000 thousand). Hii, ikiwa ni pamoja na ada ya kugaramia wahadhiri waliosahihisha insha hizo.
Bwana Chansela, kwa niaba ya Chuo Kikuu cha Egerton, ninakushukuru sana.
- Ujumbe wangu wa nane na wa mwisho, ni kuwatakia nyote mlio hapa kila la kheri na baraka zake Mwenyezi Mungu, popote pale mtakapoenda. Kwa wanaofuzu, nendeni kwa amani na muwe mabalozi wema wa Chuo Kikuu cha Egerton, mkawahudumie wananchi kwa moyo wa kujitolea, kwa heshima kuu na unyenyekevu mkiwaangazia kutokana na masomo yenu, kote nchini.
Kila la kheri na kwaherini ya kuonana. Mwenyezi Mungu Awabariki.
Ahsanteni sana!!